Kutana na mwanamke aliefanikiwa kwa kushona na kupiga rangi viatu.

45678928 - elegant men's shoes made to measure
Sikitu, ni miongoni mwa wanawake warembo, jasiri na wachapa kazi anayependa kazi yake ambaye amegoma kuajiriwa kwa kuwa anaamini kujiajiri ndiko kwenye faida zaidi kuliko kuajiriwa.

Mwanamama huyo, kwa wanaomjua hawatabisha kuhusu ujasiri wake na jinsi anavyopenda kazi yake hiyo ya kupiga rangi viatu na kutengeneza viatu vile vilivyofumuka au kukatika pamoja na kufanya ujasiriamali mdogo wa kuuza vocha za simu za mkononi na vitu vidogo vidogo kwenye eneo lake la kazi.

Anapatikana  Dar es Salaam maeneo ya Buguruni, Rozana,  biashara yake iko pembeni na baa ya Malta.

Kwa Sikitu, yeye kifo cha baba yake mzazi kilichotokea mwaka 2002, akiwa kidato cha pili, kilikatisha ndoto zake za kuendelea zaidi kimasomo.

“Mimi ni mzaliwa wa Mwanga- Moshi, Kilimanjaro, baba yangu ni mtu wa Musoma na mama yangu ni mtu wa Moshi, familia yetu ilikuwa inaishi Mwanga na tuko watoto saba kwenye familia, yetu, ila kifo cha baba yangu kilichotokea ghafla, kilikuwa pigo kwangu na wadogo zangu, ikawa ndio mwisho wa kusoma”, anasema Sikitu.

Sikitu alichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Serikali ya Vudoi wilayani Mwanga, alisoma hadi kidato cha pili na ndipo ukawa mwisho wake kwa kuwa hakupata mtu wa kumuendeleza kwa kumlipia karo ya shule.

Image result for shoe repair

Baada ya kufika Dar es Salaam mwaka 2004, alipata kazi ya upishi kwenye nyumba ya kulala wageni eneo la Mabibo, kazi aliyoifanya kwa muda kisha akapata kazi nyingine kwenye hoteli moja maeneo ya Manzese ambayo nayo aliifanya kwa miezi sita na kuamua kuacha.

“Nilifanya kazi hiyo kwa muda kidogo tu, niliona bado sijafika pale nilipotaka, kwa sababu sikupenda kuajiriwa, kwani mshahara siku zote wa kuajiriwa haitoshelezi mahitaji, hivyo nikaona ni bora nijiajiri”, alisema Sikitu.

Hapo ndipo akaanza kutimiza malengo yake kwa kuanzisha genge linalouza vitu vidogovidogo vya nyumbani maeneo ya Mabibo kwa miaka mitatu.

“Baadaye nilipata mume ambaye tunaishi naye hivi sasa na tumejaaliwa mtoto mmoja aliyezaliwa mwaka 2010”, anasema Sikitu. Baada ya kuolewa, alianza kufanya biashara na mumewe kwenye eneo la Rozana ambapo mumewe alikuwa ameshaanza ambapo alikuwa na sehemu anapiga rangi viatu na kuuza maji, juisi na vocha za simu.

Image result for black women repear shoes

“Siku nyingine wateja wa kusafisha viatu walikuwa wakija kwa wingi, wanamkuta kijana wangu ana kazi, na wakati mwingine labda nimemtuma hivyo naona waziwazi fedha hiyooo imeondoka, nikasema nitajifunza kupiga rangi na kushona viatu”, anasema Sikitu.

Kadri siku zilivyosonga, ndivyo alivyokuwa na shauku ya kujua kazi hiyo ya kupiga viatu rangi na kushona, hivyo akajifunza kupitia kwa kijana wake wa kazi na akaweza, jambo ambalo awali baadhi ya watu walikuwa wakimshangaa kufanya kazi inayofanywa na wanaume.

“Walinishangaa na wengine wakadhani ni utani, ila mimi nikasema ninafanya kazi halali sioni aibu, kwani aibu ndiyo itanifanya niwe masikini, mimi sitaki umasikini, kwa sababu najua hali ya maisha yangu na ndugu zangu”, anabainisha Sikitu.

Anasema kazi hiyo aliianza rasmi kufanya mwenyewe kwa kuanzisha eneo hilo jingine ambapo pale pa awali amemwachia kijana wake aendelee na yeye amehamia upande wa pili kwenye hiyo baa ya Malta.

Image result for black women repear shoes

Akizungumzia jinsi mumewe alivyoona kazi hiyo, Sikitu anasema, mwanzoni alipata changamoto kutoka kwa mumewe lakini alimshawishi na kumwambia yeye anachofanya ni biashara halali hivyo amuamini na kwamba wakati mwingine akiwa kwenye eneo lake la kazi mumewe alimfuata kwa siri na kukaa mahali akiangalia jinsi anavyofanya kazi zake.

Hata hivyo baada ya kuona mkewe yuko makini na kazi yake alianza kumuelewa na kumtia moyo na ndipo Sikitu akaendelea na kazi yake ambayo anasema anaipenda na hataki kuharibu kwani imempa faidi nyingi. Kwa siku moja Sikitu hupata zaidi ya wateja hata 20, wenye mahitaji tofauti, wengine ni kuosha viatu, kushona na vingine ni vya kupiga rangi.

“Mimi niko tofauti na wapiga rangi viatu wengine, napiga rangi kwa Sh 1,000 badala ya 500 ambayo wengine hutoza na nimefanya hivyo kwa kuwa kazi yangu naifanya kwa uaminifu na kwa kiwango cha juu na wateja wangu ni wengi,” anasema.

Anasema awali walikuwa wakishangaa kama kweli mwanamke anaweza kushika viatu na kufanya kazi hiyo, kwani imezoeleka kufanywa na wanaume na kwamba awali wateja walikuwa wanamuuliza “unaweza kweli kazi au? Na yeye alijibu “nipe kazi kama nitaharibu usilipe na kama nitaharibu viatu vyako nitavilipa”, aliwaambia kwa kujiamini na hapo ndio ukawa mwanzo wa yeye kupata wateja lukuki.

Hivi saa amejijengea jina katika baa hiyo na kwamba wateja wake wengine huja na furushi la viatu na kuviacha kisha kwenda kazini na kuvipitia jioni ambapo hukuta kazi yao tayari na hiyo ndio kigezo cha kujenga umaninifu kwa wateja wake.

Sikitu anasema jambo kubwa analolifanya ni kujenga uaminifu kwa wateja wake, kuwa mkweli na kufanya kazi vizuri na pia kusafisha viatu vizuri badala ya kuvilipua kama ambavyo baadhi ya wenzake wanaofanya kazi kama hiyo wanavyofanya.

Pamoja na kufanya kazi hiyo pia anauza vocha, na vitu vidogo kama leso, sigara na mifuko ambapo fedha anayopata huizungusha kwenye vikundi vya ujasiriamali ambacho kila baada ya miezi miwili hupokea Sh 900,000 na kuzifanyia biashara ambapo faida yake ni kubwa.

 

Mafanikio Kazi yake hiyo ya kupiga rangi viatu imemnufaisha , kwani hivi sasa kwa ushirikiano na mumewe wamefungua baa mkoani Dodoma na mtaji wake umetokana pia na baadhi ya faida ya kazi yake na pia hivi sasa amepata eneo ambalo kwa siku za usoni anafungua duka la jumla la mauzo ya soda.

 

“Tuache uoga, tuwe jasiri kazi unayoipenda ifanye kwa moyo utaona faida zake kama mimi nilivyofanikiwa na nimewasaidia wengi wanaonifuata na kuniuliza umewezaje, nami nawaelekeza kutimiza ndoto zako kwa kile unachopenda kukifanya, tena kifanye kwa moyo”, anamalizia Sikitu.

 

You may also like...

WP Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com