Aliacha Kazi ya Kushona Viatu na Kujitosa kwenye Biashara ya ukuzaji na Uuzaji wa Miche, Sasa ni Milionea Mtarajiwa Mjini Nakuru.

Bw Charles Macharia, almaarufu kama Ndarugu miongoni mwa wakazi wa kaunti ya Nakuru anajizatiti kulinda himaya ya mkuzaji bora zaidi wa miche kwa kipindi cha miaka 17 sasa.

Mjasiriamali huyu mwenye umri wa miaka 47 alianza upanzi wa miche mwaka 2000 ila hakutarajia mafanikio ambayo ameyapata kutokana na uamuzi huo. Akiwa moto alipanda miche kumuiga babake tu, hakujua angepata kitita kizuri kutokana na miti.

 

“Mimi kutoka utotoni nilipenda sana kupanda miti. Kabla ya wazo la kuunda pesa kutokana na miti, nilikuwa napanda miche kisha kuwapa jamaa, marafiki na majirani wapande bila kuwalipisha hata senti moja,” akasimulia.

Image result for GARDEN VEGETABLE

Je, aliwekeza pesa kiasi gani ili kuweza kujiunga na mamilionea? “Nilikuwa na KSh.25 kutokana na biashara yangu ya ushonaji viatu. Mwanamke fulani alitambua ari yangu ya kupanda miche lakini akashangaa mbona nilizidi kuwashonea watu viatu.

Alinionyesha mahali ambapo watu walikuwa wakinunua miche ya mboga kwa ajili ya kuuza. Nilipotambua hili, siku iliyofuata niliamka asubuhi na mapema na kwenda kunua miche.

Sh.25 pekee

Nilinunua miche 60 ya sukuma wiki kwa Sh10, 60 ya mchicha kwa bei hio hio na 30 ya kabichi kwa Sh5. Nilifulululiza moja kwa moja hadi sokoni Nakuru na kuuza kila mche kwa Sh1. Nilitia mfukoni Sh150,” akaelezea.

Kupanua biashara

Baada ya kuvuna faida ya asilimia 500 siku hiyo hakusita kupanua biashara yake. Alimwomba kakake baiskeli ya kusafirishia miche hadi sokoni kabla ya kuanza kukuza miche mwenyewe na kununua baiskeli yake.

Biashara hii aliifanya kwa miaka mitatu akiingiza faida ya Sh3,000 kwa siku kwani sasa wateja walikuwa wanakujia miche wenyewe kwenye shamba. Aliwaajiri wafanyakazi 2 waliomsaidia katika shughuli za upanzi na utunzaji.

Ni ufanisi huu ambao ulimwezesha kununua ploti ya kwanza mwaka 2003 kwa Sh33,000 ya futi 40 kwa 80.

Hapo sasa ndipo alipanua biashara na kuongeza upanzi wa miche ya maua, mboga, matunda, miti ya kivuli na miti ya kupasua mbao. Pia alipanua eneo alilokuwa akikuzia miche hadi ekari moja na sasa kuanza kuwauzia wateja vyungu vya kupanda maua.

Image result for VYUNGU VYA MAUA

Mwaka 2005 hakuwa na sababu ya kutomiliki lori ndogo la kuwasafirishia wateja wake miche hadi nyumbani au mahali waliponuia kuipanda.

Aliongeza idadi ya wafanyakazi wa kudumu hadi 8 huku kila mmoja akienda nyumbani na Sh300 kila siku. Mkewe, Bi Macharia ndiye husimamia kazi zote za upanzi na utunzaji miche.

Kufikia sasa  Macharia amepanda zaidi ya miche milioni 10 huku wakati wowote katika shamba lake pakiwa na miche milioni 2.

Sh200,000  kwa siku

Katika msimu wa mvua ambapo watu wengi hupanda miti, Bw Macharia hutia mfukoni Sh200,000  kwa siku huku katika nyakati za kiangazi akipata Sh10,000.

“Hakuna siku naweza kuenda nyumbani bila Sh10,000. Hapo awali nilikuwa nauza miche karibu yote na kuanza kujikuna kichwa nitakachowaambia wateja wengine wakija. Hivyo, sasa huwa napanda miche kila baada ya wiki ili niwe na viwango tofauti vya miche inayokua,” akasema.

Bei ya kila mche ni kati ya Sh1 na Sh5,000 kulingana na aina na muda wa kukua. Bei ya kila mche wa sukuma wiki, kabichi, mchicha, biringani, pilipili hoho, kitunguu, nyanya, mgongwe, koliflawa na tini (beetroot) ni Sh1.

Image result for GARDEN VEGETABLE

Bei ya mche wa Traveller’s palm ni Sh2,000, Italian Cypress Sh1000, Rubber Sh1000, Arcaria Sh800, Bamboo Sh500, Thika Palm 350, American Cypress 350, Phoenix palm 350, Umbrella Taminalia Sh300, Carnation 150, Nandi Flame Sh100, maua ya Rose Sh100(aina 6), miongoni mwa miti mingine.

Nayo miche ya mwembe, mparachichi, mtomoko, mchungwa, mlimau, mndimu, mpapai, mpera, mkarakara(passion), mzabibu, mmandala (strawberry) huuzwa kati ya Sh50 na Sh4000. Vyungu vya kupanda miche ya maua utavipata kwa kati ya Sh120 na Sh4,000 kulingana na kimo na umbo.

“Katika mwisho wa kila mwezi huwa nimeunda faida isiyopungua Sh500,000 kutokana na miche. Watu wengi wanaponitazama huona miche tu, huniita ‘mtu wa miti’,” Bw Macharia akasema huku tabasamu imemjaa usoni.

Image result for GARDEN VEGETABLE

Kupamba majengo

Kando na uuzaji wa miche, Bw Macharia hupata donge nono kutokana na huduma za kutengenezea watu binafsi, mahoteli na kampuni mbalimbali vijishamba vya kukuza miche huku akiwapambia mazingira.

“Watu binafsi hunilipa Sh400,000 kwa kazi yote huku mahoteli na kampuni nikiwalipisha hadi Sh800,000. Mimi sihitaji kuamka asubuhi nikielekea kwa ofisi ya mtu!” akasema.

Kulia kivulini

Kutokana na juhudi zake, Bw Macharia kwa sasa ameweza kununua ploti 9 ambapo mojawapo ni shamba analofuga ng’ombe wa maziwa, mbuzi na kuku wa kienyeji kwa manufaa yao ya mbolea ya kupanda miche.

Kwa sasa anamiliki lori aina ya Mitsubishi Canter ya kusafirishia wateja miche pamoja na gari lingine aina ya Toyota Lexus analotumia katika ziara zake za kaunti ndogo zote 11 za Nakuru.

You may also like...

WP Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com